Ulinzi na Usalama

Muhtasari

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa mfumo wa muundo wa Jeshi la Tanzania, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa ina wajibu wa kuhakikisha kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linasaidia na kulinda nchi dhidi ya maadui wote wa nje na kusaidia mamlaka ya raia na nguvu ya raia. JWTZ lilianzishwa mwaka 1964 baada ya maasi yaliyosababisha kuvunjwa kwa jeshi lililotokana na wakoloni, Tanganyika Rifles(TR).

Rais Nyerere aliamua kujumuisha JWTZ kwenye mfumo wa siasa na kwenye jamii inayoitumikia. Maofisa wa kijeshi na viongozi wa kisiasa walibadilishana nyadhifa jeshini, kwenye chama na Serikali. JWTZ lilikua jeshi la ulinzi na miongoni mwa majeshi ya taifa yaliyosaidia harakati za ukombozi.  JWTZ imesaidia Sera za nchi za nje na ulinzi. Tanzania kwa kushirikiana kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika na mafunzo ya majeshi ya ukombozi katika ulinzi wa nchi kutokana na ukosefu wa usalama katika mipaka na Uganda na mpaka wa Msumbiji. Kusudio la kuanzishwa Jeshi la Mgambo lilikua kujenga dhana ya uwajibikaji na fahari ya nchi kwa wananchi kwa kuwakaribisha raia nao washiriki katika ulinzi wa nchi.

Jeshi la kujenga Taifa (JKT) lilianzishwa ili kuwawezesha vijana wa Tanzania kujenga umoja wa kitaifa na kuhudumia nchi. JKT huwapa vijana mafunzo ya kijeshi na stadi za kujitegemea. Jeshi la Kujenga Taifa na Mgambo hulipa JWTZ jeshi la akiba kuongeza uwezo na nguvu za kijeshi.

Uzalishaji Mali kupitia Viwanda

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limekuwa likijihusisha na shughuli za uzalishaji mali kupitia viwanda vyake kwa kutumia wataalamu wanajeshi na watumishi wa umma. Jeshi limekuwa likizalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo zana za kilimo, mashine mbalimbali, malighafi zinazotumika katika ujenzi, kupitia viwanda na mashirika yake, kama Shirika la Uzalishaji mali la Jeshi la kujenga taifa (SUMA JKT), Shirika la Mzinga lililopo Mazao Mkoani Morogoro, Mradi wa Nyumbu uliopo Kibaha Pwani, Kiwanda cha kushona kilichopo Ruvu JKT.

Nifanyeje kujiunga na JWTZ?

Uandikishaji

  • Mtu yeyote ataandikishwa kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa sifa zifuatazo: -
  • Awe raia wa Tanzania
  • Awe na Elimu ya kidato cha nne na kuendelea na awe amefaulu..
  • Awe hajaoa/hajaolewa
  • Awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 25
  • Awe na tabia na mwenendo mzuri
  • Awe na akili timamu na afya nzuri

Masharti ya Utumishi

  • Askari atapewa nambari ya utumishi baada ya kufaulu mafunzo ya awali.
  • Atalitumikia Jeshi kwa kipindi cha mwanzo cha miaka sita, baada ya hapo atafanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili miwili kwa kibali cha Mkuu wa Majeshi.

Maafisa

Bodi ya Uteuzi wa Maafisa (Officers Selection Board) huwafanyia usaili Askari wenye elimu ya kidato cha sita na kuendelea toka Vikosini na Shule za Askari wapya (Recruitment Schools).

Watakaofaulu masailiano hayo hupewa hadhi ya Afisa Mwanafunzi (Officer Cadet), na hupelekwa Chuoni (Tanzania Military Academy) kwa mafunzo ya Uafisa kwa muda wa mwaka mmoja.  

Siku ya Mashujaa

Tanzania huadhimisha Siku ya Kuwakumbuka Mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda uhuru wa Tanzania kila ifikapo Julai 25 ya kila mwaka. Siku hii ya kuwakumbuka mashujaa huambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalum ya kuwaombea mashujaa waliopoteza maisha na kuiombea amani nchi kutoka kwa viongozi wa dini. Pamoja na hayo hufanyika gwaride maalum kwa ajili ya mashujaa wetu.

Siku ya Majeshi

Tarehe 01 Septemba ya kila mwaka JWTZ husherehekea sikukuu ya Majeshi ikiwa ni ishara ya kuanzishwa kwake. Sikukuu ya Majeshi huwapa fursa ya kipekee Wanajeshi kufanya kazi mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za afya bure kwa wananchi, kushiriki katika michezo mbalimbali, kufanya usafi katika maeneo ya wazi na yale ambayo hutumiwa na wananchi kama vile masoko na vituo vya usafirishaji. Hayo yote hufanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuanzishwa kwa JWTZ.

Mpangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi