Mazingira

Vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2023/24

  1. Kusimamia Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2032) na kuchukua hatua za kupunguza uharibifu wa Mazingira
  2. Kuimarisha usimamizi wa Biashara ya Kaboni nchini
  3. Kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, 55 Mabadiliko ya Tabianchi na Fursa ya Biashara ya Kaboni
  4. Kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira 2021 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 ikijumuisha utoaji elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya Sheria na Sera ya Mazingira
  5. Kuratibu utekelezaji wa Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira

Miradi ya kitaifa inayopunguza uharibifu wa mazingira

  1. Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa itakayotumia umeme badala ya mafuta ya dizeli na hivyo kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa
  2. Mradi wa kuzalisha umeme wa maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere utakaochangia umeme kiasi cha megawati 2,115 kwenye gridi ya taifa na hivyo kupunguza uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta mazito yanayoharibu mazingira
  3. Mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam 19 unaochangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa kupunguza idadi ya magari yanayotumia mafuta ya dizeli na petrol
  4. Mradi wa usambazaji wa nishati ya gesi majumbani na kuweka vituo vya kujazia gesi kwenye magari katika Jiji la Dar es Salaam; na programu ya nishati safi ya kupikia.

 

Maendeleo endelevu ya Uchumi wa buluu

Nchi ya Tanzania imejaliwa kuwa na ukanda mrefu wa pwani wa takribani kilomita 1,450 na Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee unaofikia kilomita za mraba 223,000. Eneo la maji linalochukua kilomita za mraba 64,000, hivyo kuifanya nchi kuwa tajiri kwa bionuai pamoja na uwezo mkubwa wa uchumi wa buluu ambao unasaidia, maisha ya mamilioni ya watu ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula na njia ya usafiri.

Licha ya Bahari kuchangia zaidi ya asilimia 50 ya Oksijeni duniani pamoja na kuwa chanzo cha ajira kwa watu zaidi ya milioni 60 na chanzo kikuu cha maisha kwa mabilioni ya watu lakini bado changamoto za uharibifu wa ikolojia ya bahari zimeendelea kuwepo ambazo zinahatarisha mfumo mkubwa wa ikolojia duniani pamoja na maisha ya watu waliowengi.

Mataifa yanatakiwa kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa manufaa ya kiuchumi kwa nchi zote ikiwa ni pamoja na kuunganisha nguvu za pamoja ,kuwekeza katika teknolojia za kibunifu pamoja na tafiti. Ni muhimu kuwashirikisha moja kwa moja makundi ya kijamii ikiwemo wanawake, vijana na jamii inayotumia bahari ili kudhibiti matumizi yasiosahihi ya bahari na rasilimali zake.

Ili kufikia maendeleo endelevu ya Uchumi wa Buluu inapaswa kuzingatia hali ya kijamii, kiuchumi na kimazingira wakati wa matumizi ya rasimali za bahari kama vile ongezeko la idadi ya watu ulimwenguni, kuongezeka kwa matumizi na hitaji la vyanzo vipya vya chakula, nishati na madini.

Tanzania itaendelea kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kurejesha mifumo ikolojia ya bahari , ikiwa ni pamoja na kutenga asilimia 6.5 ya sehemu ya bahari ya Hindi kuwa Maeneo Tengefu ya Bahari, kudhibiti uvuvi haramu kwa karibu asilimia 99 pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.

Matumizi endelevu ya Maji

Maji ni rasilimali muhimu katika kila nyanja ya maisha na maendeleo ya mwanadamu na taifa kwa ujumla.  Hali hii inasababisha mataifa yetu kutaka kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji ya kutosha. Kutokana na umuhimu wa kipekee wa rasilimali maji, usimamizi wa rasilimali hii ya pamoja (shared water resouce) unahitaji umakini, utashi mkubwa na kuaminiana katika kutafuta namna bora ya matumizi yake, ambapo kinyume na hilo, tunaweza sababisha migogoro baina yetu.

Katika bara la Afrika, vita na migogoro kadhaa imekuwa ikijitokeza kutokana na kugombania rasilimali ikiwemo rasilimali maji. Hii imesababisha wengi kujiuliza endapo rasilimali hizi ni laana au faida kwa bara la Afrika. Hata hivyo, yafaa kukumbuka kwamba kuna mabara mengine ambayo yameweza kutumia rasilimali ikijumuisha rasilimali za pamoja kama mito kuwa chanzo cha amani na maendeleo!

Hii ina maana kuwa, ushirikiano kwenye matumizi ya rasilimali za pamoja unawezekana. Inabidi tuendelee kudumisha na kuendeleza umoja wetu katika usimamizi, uendelezaji na matumizi endelevu kwa faida yetu sote.

Panda Mti, Tunza Mazingira

Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ina dhamana kubwa ya kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kijani na yenye mazingira safi. Ingawa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya bustani za kupumzikia (green parks) tayari yamevamiwa na wananchi wamejenga. Sheria ndogondogo kuhusiana na suala zima la hifadhi na usimamizi wa mazingira inabidi ziwekwe bayana na kusimamiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na faini na adhabu mbalimbali zitakazohusika.

Zoezi la kutunza mazingira kwa ajili ya maendeleo ni zoezi shirikishi linalohusisha jitihada za pamoja kutoka Serikali Kuu, serikali za mitaa, taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali; Sekta Binafsi; wadau wengine na jamii nzima, kuanzia mijini hadi vijijini zote kwa pamoja. Wizara na taasisi zote za Serikali zinatakiwa kupanda miti na kutunza mazingira katika maeneo yao yanayowazunguka.

Zoezi hili linapaswa kufanyika katika kila kaya; shule zote kuanzia msingi hadi vyuo vikuu; kwenye maeneo ya taasisi za dini kote nchini; kwenye maeneo yanayomilikiwa na taasisi binafsi kama vile vituo vya kuuza mafuta; na pia kwenye maeneo ya viwanda. Aidha, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara vijijini (TARURA) pia wanatakiwa kuhakikisha wakandarasi wanapanda miti na maua pembezoni mwa eneo la akiba la barabara (road reserve) kwa kila barabara mpya inayojengwa pia uwekaji wa taa za barabarani na barabara za watembea kwa miguu. 

Vyombo vya ulinzi na usalama vinatakiwa kuhakikisha upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira katika maeneo yote nchini.  Vyombo vya ulinzi na usalama vinatakiwa kuwa mfano bora katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika maeneo yanayowazunguka ikiwa ni pamoja na barabara kuu zinazopita pembeni au ndani ya Kambi.

Vitendo vingi vinavyosababisha uharibifu wa mazingira nchini vinafanywa bila kujali athari zake katika jamii . Vitendo hivi ni pamoja na ukataji wa miti hovyo; uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu; uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu. 

Halmashauri za Miji, Serikali za vijiji na mitaa kote nchini zinatakiwa kuweka mikakati ya kukomesha uchomaji moto ovyo na kuhakikisha wanarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili katika maeneo ambayo miti ya asili iko kwenye tishio la kutoweka.

Serikali inatambua mchango wa Sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na washirika wa maendeleo na nchi rafiki katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye suala la kuhifadhi mazingira. Viwanda nchini, vinapaswa kuendelea kuzingatia misingi ya uzalishaji endelevu, matumizi ya mbinu bora za uzalishaji na teknolojia rafiki kwa mazingira. Vilevile, kuongeza juhudi hasa katika kuhamasisha, kukuza uelewa na kujenga uwezo wa jamii na taasisi mbalimbali kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kupitia wataalam, teknolojia na rasilimali fedha.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004

Bonyeza hapo chini kupata Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004

https://www.vpo.go.tz/uploads/files/SHERIA-YA-MAZINGIRA.pdf

Mpangilio