Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani

Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani 2022 .

Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuwasaidia Wajane nchini kuondokana na kero kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo baada ya kufiwa na wenza wao.

Serikali inatambua kwamba Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani ni jukwaa linalowaleta pamoja wajane na kuwapa fursa ya kushiriki na kubaini changamoto wanazokumbana nazo na hata kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. .

Tanzania huadhimisha Siku ya Wajane kwa lengo la kukuza hamasa, mshikamano na uelewa ndani ya jamii ili kuacha ukiukaji wa haki za binadamu kwa wajane. Hivyo, kama Taifa, maadhimisho haya yanatoa fursa ya pamoja katika kubaini changamoto za wajane na namna ya kukabiliana nazo .

Miongozo ya Mabaraza ya Watoto na uanzishwaji wa Madawati ya Watoto

Miongozo ya Mabaraza ya Watoto na uanzishwaji wa Madawati ya Watoto katika Shule za Msingi na Sekondari imezinduliwa Siku ya Mtoto wa Afrika ikiwa ni hatua muhimu katika kukabiliana na kadhia ya ukatili kwa kundi hilo ndani ya jamii. Kuzinduliwa kwa miongozo hiyo ni hatua muhimu katika kusukuma ajenda ya kupinga ukatili hususan kwa kundi hilo la watoto.

Watoto nchini wamekuwa wakipitia ukatili mbalimbali ikiwemo wa mitandaoni, hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau na imeandaa miongozo kwa Wanafunzi, Walimu pamoja na Wazazi ili iwe msaada katika malezi na makuzi ya watoto wetu” alisema Dkt. Gwajima.

 Serikali kupitia Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 inatambua Haki tano (5) za Msingi za Mtoto ambazo ni Haki ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na haki ya Kutobaguliwa hivyo kuzinduliwa kwa mongozo ni chachu ya kuongeza mapambano ya kumlinda Mtoto. Miongozo hiyo itapelekwa kwenye Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Vyuo vya kati, kwenye Madawati ya ulinzi wa Mtoto na Mabaraza ya Watoto ambayo yanakwenda kuanzishwa nchi nzima ili iwe ni fursa kwa watoto kujadiliana na kueleza madhila yanayowasibu.

Serikali pamoja na Wadau baada ya tafiti zake waliona umefika wakati kwa watoto kupatiwa Miongozo itakayowasaidia uendeshaji wa Mabaraza yao. Wazazi na walezi kote nchini wanatakiwa kuwaruhusu watoto kujiunga na kushiriki katika mabaraza ya Watoto ili kutoa fursa kwa wao wenyewe kubainisha changamoto zinazowakabili.

Chimbuko la Siku ya Mtoto wa Afrika ni azimio la Umoja wa nchi za Afrika (OAU) la mwaka 1991 lililokuwa na lengo la kuwaenzi Watoto kutoka shule mbalimbali za nchini Afrika Kusini hususani Kitongoji cha Soweto waliouawa kinyama na Polisi wa Serikali ya Makaburu tarehe 16 Juni,1976. Watoto hao wanaokadiriwa kufikia 2000 waliuawa wakati wanaandamana kupinga elimu ya kibaguzi dhidi ya watoto wenye asili ya kizungu.

Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, 2022 (SMAUJATA)

Wizara kwa kushirikiana na wadau wake zikiwemo Wizara mbalimbali za kisekta inaratibu kampeni shirikishi ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi wote kuungana kupinga vitendo vya ukatili wa aina zote kwenye jamii ijulikanayo kama SMAUJATA (Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, 2022). Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mkoani Dodoma. Dhana ya Kampeni hii ni kuandikisha wanachama wengi zaidi kutoka ngazi zote na mitandao yote ya jamii wanaokerwa na uwepo wa ukatili, wenye moyo wa kujitoa bila ujira wowote kwenye kuelimisha jamii ili ifahamu juu ya uwepo wa ukatili na athari za ukatili na hatua gani wachukue kabla ya ukatili kufanyika na pale ambapo umefanyika.

Kampeni hiyo ya SMAUJATA ni shirikishi kwa lengo la kuongeza nguvu na kasi ya kupambana kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto na kwenye jamii kwa ujumla. Kampeni hiyo imepokelewa kwa mtazamo chanya ambapo hadi sasa wananchi zaidi ya 5000 wameshajiunga.

Pamoja na jitihada mbalimbali za kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa watoto, bado taarifa za vitendo hivyo hususani kwa watoto zinaendelea kuongezeka ikiwemo Ubakaji, Ulawiti, Utumikishwaji wa watoto katika ajira hatarishi, Ukeketaji, Ndoa na mimba za utotoni na vitendo vingine vya ukatili. Licha ya watuhumiwa wa ukatili kuchukuliwa hatua kali za kisheria Takwimu za Jeshi la Polisi, zinaonesha idadi ya matukio inashamiri.

Kulingana na takwimu za Polisi Tanzania katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2021 jumla ya matukio ya ukatili kwa watoto yaliyoripotiwa katika jeshi la Polisi ni 11,499 ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020 (upungufu ni matukio 4,371 sawa na asilimia 27.5).

Mikoa iliyoongoza kwa vitendo hivyo ilikuwa ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489). Aidha, makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na ulawiti (1,114). Kwa upande mwingine, utafiti wa serikali na UNICEF unaonesha asilimia 60 ya matukio yanatokea nyumbani na asilimia 40 yanatokea mashuleni.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika nchini yamefanyika kwenye ngazi za Mikoa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum iliuungana na Mkoa wa Dodoma katika Viwanja vya Nyerere Square.

Mpangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi